ebook img

kumkumbuka allah PDF

51 Pages·2012·1.7 MB·Swahili
Save to my drive
Quick download
Download
Most books are stored in the elastic cloud where traffic is expensive. For this reason, we have a limit on daily download.

Preview kumkumbuka allah

KUMKUMBUKA ALLAH (DHIKR - E ILAAHI) HOTUBA ILIYOTOLEWA NA HADHRAT MIRZA BASHIRUDDIN MAHMOOD AHMAD (RA) KHALIFAT-UL- MASIH II _______ Mfasiri: MUSA A. MPINGA - DAR ES SALAAM KUMKUMBUKA ‘ALLAH’ (Dhikr-e ilaahi) Napenda kuelezea masuala yafuatayo:- - Dhikr-e -ilaahi au kumkumbuka Allah ni nini? - Kwa nini Dhikr-e -ilaahi ni muhimu? - Namna mbalimbali za Dhikr-e -ilaahi - Tahadhari za kuchukua katika kufanya Dhikr-e -ilaahi - Makosa ya kawaida ya uelewa kuhusu Dhikr-e -ilaahi - Njia za kukomesha athari za shetani na kuendeleza umakini katika sala Somo hili lina umuhimu mpana. Linawahusu binadamu wote, wa juu na chini, matajiri na masikini, wachanga na wazee. Pale utakapotekeleza kwa matendo mawazo ninayokusudia kuyatoa leo, matokeo yenye manufaa ya Dhikr-e -ilaahi yatakuwa bayana. Dhikr-e -ilaahi au kumkumbuka Allah ni nini? Dhikri, ni neno la kiarabu, maana yake ni kukumbuka. Pale linapotumika kumhusu Allah, linamaanisha njia za kumkumbuka Allah, kuweka sifa zake akilini, kuzitaja tena na tena, kuzikubali kwa hamu na ukweli wa moyo, na kutafakari juu ya uweza wake na nguvu yake. Umuhimu wa mada hii Dhikr-e -ilaahi ni muhimu kiasi gani? Kwa kifupi somo hili ni nyeti na ni la umuhimu mkubwa. Sisemi umuhimu mkubwa kwa sababu ya kauli tu, bali kwa sababu Allah Mwenyewe Ameliita hivyo. Allah Anasema; Na kwa yakini kumbuko la Allah ni (jambo) kubwa kabisa. (Kurani Tukufu 29:46). Yaani kumkumbuka Allah kuna daraja la juu zaidi kuliko matendo mengine yote ya ibada. Kwa hiyo kauli ya kwamba somo hili ni la muhimu sio yangu mimi, ni tamko la Allah Mwenyewe. Kwa nini Dhikr-e-illahi ni jambo la lazima? Kama suala ni la umuhimu mkubwa kiasi hiki, ni dhahiri Islam itaweka mkazo endelevu juu yake. Na hivi ndivyo hasa ilivyo. Tunaona ukumbusho wa mara kwa mara juu ya jambo hili katika Kurani Tukufu, kwa mfano:- Na likumbuke jina la Mola wako asubuhi na jioni (76:26) Hali kadhalika kuna Hadithi ambamo Mtume Mtukufu (saw) amesema; “Pale watu wanapokusanyika pamoja kwa ajili ya kumkumbuka Allah, wanazungukwa na malaika na kufunikwa na rehema kutoka kwa Mola. Hii ndiyo sababu ya kuchagua mada hii kwa ajili ya mkutano wa mwaka. Maelfu kati yenu mmekuja kutoka mbali sana ili kuhudhuria mkusanyiko huu. Nitakapokuwa naelezea mada hii, malaika watakuwa wanawamiminieni rehema za Mungu. Mtakaporejea nyumbani na kuyafikisha mliyoyasikia, wasikilizaji watapata rehema, na kwa jinsi hii rehema zitawafikia Wanajumuiyya wote. Hadithi niliyoitaja mapema inaonyesha kwamba kumkumbuka Allah katika mkusanyiko ni jambo la baraka. Linavutia malaika ambao pamoja nao, huja na rehema na msaada wa Allah, kwa hiyo umuhimu wa Dhikri wapaswa kuwa wazi. Bila shaka malaika watamuauni mtu ambaye kwa kufanya kwake Dhikri, anavutia upamoja nao mara kwa mara, na kila mara atakumbushwa nao kutenda matendo mema. Kuwepo kwa malaika sio utungo wa fikra ya kibinadamu, bali ni ukweli. Mimi Mwenyewe ninawaona malaika. Nilipata mara moja kuongea nao kirafiki kabisa. Kwa kuja kwao mara kwa mara, malaika hujenga mapenzi na urafiki na wale wamkumbukao Allah. Mwenyezi Mungu Anasema; Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu wala watoto wenu kumkumbuka Allah (63:10). Enyi mlioamini, mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na mtukuzeni asubuhi na jioni. (33:42 - 43) Mtume Mtukufu (saw) ametilia mkazo umuhimu wa Dhikri katika hadithi zake. Hadhrat Abu Musa Ash’ari anasimulia kwamba Mtume Mtukufu (saw) anasema, “Mfano wa mtu anayemkumbuka Mola wake na yule asiyemkumbuka, ni kama aliye hai na mfu”. Yule amkumbukaye Allah yuko hai, na yule asiyemkumbuka amekufa”. Hadhrat Abi Darda’a anasimulia ya kuwa Mtume Mtukufu (saw) amesema, “Je nikuambieni juu ya tendo jema na takatifu kabisa hata kwa wafalme, ambalo huinua daraja lenu, ambalo ni bora zaidi kuliko kutoa dhahabu na madini ya fedha, ambalo ni bora zaidi kuliko kukutana na maadui na kukata shingo zao, au ninyi wenyewe kuupata ushahidi? Masahaba wakajibu, Naam, tueleze tafadhali. Mtume Mtukufu (saw) akasema; “Ni kumkumbuka Allah”. Sawa na Hadithi nyingine Mtume Mtukufu (saw) amesema; kumkumbuka Allah kuna malipo makubwa. Masahaba wakauliza, Ewe Mjumbe wa Allah, jambo hili ni bora kwa malipo kuliko kujitahidi katika njia ya Allah? Akajibu ndio, kwa vile ni kumkumbuka Allah ndiko kunakomhimiza mtu kuifanya hiyo juhudi. Haja ya kuzingatia kwa mkazo zaidi Dhikri katika Jamaat yetu. Huo ndio umuhimu wa Zikri. Hata hivyo, kwa namna fulani baadhi ya Wanajumuiyya wa Jamaat yetu hawatilii mkazo jambo hili. Mungu Mwenye Enzi Ameielekeza fahamu yangu katika kutafakari na kuliwazia jambo hili. Nimewaza juu ya jambo hili tangu nikiwa kijana mdogo na hadi leo nafikirishwa na jambo hili kama nilivyokuwa wakati ule. Uvivu wowote uliopo katika Jamaat yetu katika kumkumbuka Allah ni lazima uondolewe. Masihi Aliyeahidiwa (as) ameweka mkazo mkubwa katika sala. Kwa msaada wa Mungu, Jamaat yetu inaangalia sana wajibu huu. Masihi Aliyeahidiwa (as) amesisitiza pia umuhimu wa kumkumbuka Allah, lakini Jamaat bado haijalipa suala hili uzito unaotakiwa. Uvivu katika kumkumbuka Mungu hutokana na athari ya elimu ya kimagharibi kwa kiasi fulani. Watu wengi wanafikiri hakuna haja ya mtu kukaa peke yake na kusema ‘Laa Ilaha Ilallah’ (Hakuna apasaye kuabudiwa ila Allah) au kutaja sifa za Mungu kama Qudduus (Mtakatifu), ‘Aliim (Mwenye elimu), Khabiir (Mwenye habari), Qadiir (Mwenye nguvu) au Khaaliq (Muumbaji). Wengi wa Wanajumuiyya wetu waliopata elimu ya kimagharibi, wameathirika na mawazo haya. Wakulima huunda kundi jingine kubwa katika Jamaat yetu. Zamani hawakuwahi kupata habari za kutosha juu ya dhana ya Dhikr na faida zake. Kwa hiyo nao wanakosa tabia ya kufanya Dhikr. Mpaka pale Jamii ya wakulima itakapopata habari za kutosha na kufundishwa vilivyo, haiwezi kutazamiwa (wao) kuzingatia barabbara kumbuko la Allah. Salat (kusali sala tano zilizopangwa katika siku) pia ni kumkumbuka Allah. Kwa msaada wa Allah Jamaat yetu inafuatilia vyema kabisa sala. Hata hivyo, kuna njia nyingine muhimu za kumkumbuka Mungu tofauti na sala. Ingawa si kwamba hazishikwi kabisa katika Jamaat, bali mkazo wa kutosha hauwekwi kwenye njia hizi. Baadhi ya Wanajumuiyya wanakosa kabisa tabia ya kumkumbuka Allah pamoja na Salat, hili ni kosa kubwa. Ikiwa mtu ni mzuri mno wa sura lakini ana macho mabovu, au masikio au pua mbaya, ataitwa mzuri? Hapana kabisa. Kila mtu atasema anachukiza. Kwa maneno mengine Mwanajumuiyya ambaye hatumii baadhi ya njia za kumkumbuka Allah ni kama mtu ambaye amevaa koti la gharama sana, shati, jacket na suruali, lakini anakosa viatu au kofia. Bila kujali nguo zake zilizoshonwa vizuri, kukosa kwake viatu au kofia kunafanya muonekano wake kuwa na kasoro. Ukosefu wa tabia ya kumkumbuka Allah ni kasoro, na watu wenye onjo zuri hawapendi kasoro yoyote binafsi. Nitathibitisha kwamba pamoja na Salat, njia nyingine za kumkumbuka Allah zimehimizwa na Allah na Mtume wake (saw). Ikiwa mtu anaelewa falsafa ya mahimizo haya au la, ni wajibu kuyafuata ili kupata maendeleo ya kiroho. Baadhi ya Wanajumuiyya wa Jamaat yetu wanadhani kwamba kwa kutimiza ibada za faradhi wametimiza wajibu wao na hakuna haja ya Nawafil, yaani sala za ziada. Hii ni dhana potofu. Mtume Mtukufu (saw) anasema kwamba Mungu Mwenye Enzi Amemuambia kuwa, kwa kusali Nawafil Mtumishi wangu anakuwa karibu mno nami kiasi ya kwamba ninakuwa masikio ambayo kwayo husikilia, macho ambayo kwayo huonea, mikono ambayo kwayo hushikia na miguu ambayo kwayo hutembelea. Hadithi hii inafichua thamani iliyopewa Nawafil na Allah, na ukubwa wa daraja la mtu anayezishika. Allah humwinua juu sana kiasi ya kwamba anaanza kuakisi sifa zake. Nawafil si jambo la kawaida, kwa hiyo kukosa kuzingatia kuzitimiza ni sababu ya masikitiko makubwa. Mwanadamu ana asili ya uvivu na kutopenda kufanya juhudi. Anatamani akabiliane na ugumu na nidhamu ndogo kadiri iwezekanavyo. Mwenyezi Mungu Ambae Anatambua udhaifu wa viumbe vyake, kwa rehema Zake, Ameteua baadhi ya matendo ya ibada kuwa faradhi na mengine kuwa ya ziada. Ibada za faradhi zinaweka kiwango cha ibada zinazomwezesha mtu kukubalika. Yeyote anayezitimiza kikamilifu anakuwa hana lawama. Imesimuliwa kwamba mtu mmoja alimjia Mtume Mtukufu (saw), na akauliza juu ya Islam. Akajibu Mtume (saw), Sala tano kila siku mchana na usiku. Akauliza, kuna Sala zozote zingine baada ya hizi? Mtume Mtukufu (saw) akajibu, hakuna mpaka wewe mwenyewe upende. Kisha, Mtume Mtukufu (saw) akaendelea; kufunga katika mwezi wa ramadhani, tena yule mtu akauliza, kuna funga zozote nyingine baada ya hii? Mtume Mtukufu (saw) akajibu hapana mpaka wewe mwenyewe upende. Kisha Mtume Mtukufu (saw) akamwambia juu ya Zakat, wajibu wa kifedha wa Waislam, yule mtu akarudia swali lile lile na akapewa jibu lile lile. Yule mtu akaondoka akisema, naahidi kwa jina la Allah sitaongeza chochote katika haya, na sitapunguza chochote. Mtume Mtukufu (saw) akasema, kama amesema kweli (kama atatimiza ahadi yake hii), ameshafanikiwa. Kwa kifupi ibada za faradhi zikifanywa kwa makini, zinahakikisha ufaulu. Lakini waangalifu na wenye busara hawajibani kwenye ibada za faradhi pekee. Wanauingia uwanja wa Nawafil ili kujazia upungufu unaoweza kuwapo katika ibada zao za faradhi. Kwa mfano sala tano kila siku zimefaradhishwa, hata hivyo kusahau au mghafiliko waweza kutokea katika mojawapo ya hizo na kuzifanya kuwa batili. Kutakuwa na wajibu utakaodaiwa siku ya malipo kwa mapungufu kama haya katika sala. Nawafil itajaziliza faradhi kama hizi. Inasimuliwa kwamba Mtume Mtukufu (saw) mara moja alimwona mmoja wa masahaba zake akisali. Akamwamuru kurudia sala, nae akarudia, lakini Mtume Mtukufu (saw) akamtaka kurudia tena mara ya pili na ya tatu. Yule sahaba akaomba Ewe Mjumbe wa Allah sifahamu namna ya kusali vyema zaidi, tafadhali nifundishe. Mtume Mtukufu (saw) akajibu, ulikuwa unaharakisha mno katika kusali, hivyo haiwezi kukubaliwa na Allah, sali pole pole na sala yako itapokelewa. Hebu nifafanue hoja hii, kwa mfano mwanafunzi anafanya mtihani ambao anahitaji maksi hamsini ili kufaulu. Ikiwa atajibu maswali yawezayo kumpa maksi hamsini tu, hawezi kuwa na hakika ya ufaulu wake. Anaweza kufeli kwa sababu mojawapo ya maswali hakulijibu sawa sawa. Au fikiria msafiri anayejiandaa kufanya safari ndefu. Anaweza kukadiria fedha zinazohitajika wakati wa safari, lakini wakati wa safari anaweza kukabiliana na dharura inayohitaji fedha zaidi. Nawafil ni kama fedha za ziada kwa ajili ya dharura. Ni za muhimu na zapaswa kupewa mkazo maalum. DHANA POTOFU JUU YA DHIKR Kuna dhana potofu iliyoenea juu ya Dhikri katika Jamaat yetu. Kwa kuwa inaonekana inapelekea kupuuzia Dhikri, nataka kuondoa dhana hii potofu. Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu Masufi (wale wajiitao Madaruweshi) wa zama zake ambao waliingiza bidaa nyingi katika Islam. Alibainisha kurudia rudia kwao kikasuku maneno mbalimbali ya Dhikr kulikuwa hakuna maana, kwani huo ulikuwa ni wakati wa kuuhami Uislam kutokana na mashambulizi ya maadui. Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu - na hili walilistahili, lakini baadhi ya Waahmadiyya walimwelewa vibaya. Dhana kwamba kukaa mahala kwa ajili ya kumkumbuka Allah hakuna maana ni potofu kabisa. Aina zote za Dhikr zakusudiwa kumsifu Allah na kuzitukuza sifa zake. Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu wale waliokuwa wanazitaja sifa za utukufu wa Mungu wakiwa wamejifungia majumbani mwao, lakini wasithubutu kuwakabili maadui waliokuwa wakimimina matusi katika jina lake tukufu. Aliwaasa kwa kuwa walikuwa waoga. Walikuwa hawatimizi wajibu wao wa kuwaita watu kwenye wema na kukataza mabaya. Matendo yao yalikuwa ni unafiki, kama wangekuwa waaminifu ki-ukweli katika kumtukuza kwao Mungu, kwa nini hawakuyakabili mashambulizi ya maadui? Kwa nini hawakumtukuza Allah hadharani kama walivyofanya katika kona zilizonyamaa za nyumba zao? Zaidi ya hayo, Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwalaumu kwa kuwa waliiharibu dhana ya Dhikr. Matendo yao hayakuwa na alama yoyote ya dhana ya kumkumbuka Mungu katika uhalisia wake. AINA ZA DHIKRI ZILIZOPOTOKA Aina kadhaa potofu za Dhikr zinapatikana kati ya Masufi. Wanalia kilio kutoka nyoyoni mwao na wanakipeleka kichwani mwao na kupiga kelele kwa sauti kiasi hiki kwamba hakuna yeyote jirani nao anaweza kulala au kumakinika katika ibada. Hii inaitwa kuupenya moyo - kama vile La ilaha ilallah itaingia nyoyoni mwao ikiwa tu itagongelewa iingie ndani. Ingawa wanasema kwamba wanakusanyika kwa ajili ya Dhikr, wanajitia tu wazimu kwa sauti tupu za Allah, Allah. Kuna matendo ya namna nyingi, mbalimbali; - Baadhi wanabarizi tu na nyimbo, vibwagizo na kucheza na wasichana makahaba, eti wanaiita hali hii kuwa ni kikao cha Dhikr kwa sababu tu neno Allah linatajwa mara kwa mara. - Wengine ‘Wanazipenya’ nyoyo zao - Wengine hutoa ukelele kutoka rohoni mwao - Wengine eti huitoa Dhikr kutoka katika nyoyo zao na inarejea baada ya kusujudu katika Arsh - Kiti cha Enzi cha Allah. - Wengine hucheza kwa kuifuata sauti ya usomaji wa Kurani Tukufu huku wengine wakirukaruka na kusoma ushairi, hujifanya wanapandisha madadi na kupoteza fahamu. Hapo ndipo mmoja wao huruka katikati ya mkusanyiko na kutoa sauti za kifuani za Allah, Allah. Kwa kifupi, mambo mengi yasiyofaa na machafu yameingizwa katika dhana ya Dhikri. Hakuna lolote kati ya hayo lenye kulandana na mafundisho ya kweli ya Islam. Tunazilaani bidaa hizi, lakini hatuwezi kuiacha Dhikr kwa sababu ya haya. Mtume Mtukufu (saw) amesema kila ubunifu (bidaa) humpeleka mtu mbali na njia ya Allah na zote hizo zinaelekeza motoni. Hii ndiyo sababu Dhikr kama hii haiwapeleki watu hawa karibu na Allah, badala yake inawaweka mbali Naye. Tangu aina hii ya Dhikr ilipoanzishwa, Waislam wameenda mbali na Allah. Hii haishangazi, matendo yaliyo kinyume na mwongozo wa Allah na Mtume wake ilikuwa ni lazima yahafifishe hali ya kiroho. Ubunifu (bidaa) wote ulioingizwa katika Dhikr una vionjo vya starehe, lakini starehe yenyewe ni ya kiini macho. Mtu anayeiangukia starehe hii na kuacha starehe ya kweli ameharibikiwa. Ni kama mtu anayeugua maumivu ya tumbo na badala ya kutafuta tiba ya kweli, anajitia usingizini kwa dawa ya usingizi. Nguvu ya kuzuia maumivu inaleta nafuu ya muda, lakini kwahakika anajiua mwenyewe. Muda utawadia upesi ambapo ugonjwa utafanya uharibifu wake. DHIKRI DHIDI YA VIINI MACHO Kile kinachoitwa Dhikr na watu hawa kwa kweli ni kiini macho na pumbazo la akili (mesmerism & hypnotism). Haina uhusiano wowote na hali ya kiroho, bali inahusiana na hudhurisho la mawazo. Mungu Mwenye Enzi Ameweka katika dhati ya mwanadamu nguvu ya kuleta athari kubwa kwa njia ya kukazia mawazo kwenye jambo fulani. Hisia za burudiko kama zile zitokanazo na madawa ya kulevya kama opium, cocaine na bangi zinaweza kupatikana kutokana na mkazio huu wa mawazo. Hisia hizi sio burudiko la kweli bali ni hali ya pumbazo. Watu kama hawa wanajidanganya wenyewe katika kuamini kwamba wanapata burudiko kwa kutaja jina la Allah. Kwa kweli hata wangetaja Ram, katika wakati ule wa kazio la mawazo hisia zao zisingekuwa tofauti. Inasimuliwa kwamba Mwislam mwenye heshima alikuwa anasafiri katika boti. Akaanza kudhikiri kwa mkazo kamilifu. Wengine, hasa Wahindu wakajiunga nae katika kusema Allah, Allah. Hata hivyo Mhindu mmoja hakuathirika, yule Mwislam akaanza kukazia mawazo yake kwa yule Mhindu na yule Mhindu nae akaanza kukazia mawazo yake kwa Mwislam kwa nguvu zaidi. Badala ya kumuathiri Mhindu, Mwislam akaathirika mwenyewe. Bila kutaka akaanza kutamka Ram, Ram. Mwislam alipigwa na butwaa na akang’amua kuwa kufanya Dhikri kwa njia hii kulikuwa sio sahihi. Alitubu na akaachana na mazoea haya. Aligundua kwamba matokeo hutokana tu na utumiaji wa ujuzi, na sio kumkumbuka Allah, kama baraka ya kutamka Allah ilikuwa ndio chimbuko la burudiko lake, kutaja Ram kusingeweza kuleta hisia ile ile. Wale wanaofanya jinadi kama hizi hali yao ni kama msafiri jangwani. Akiona kapu limejaa mchanga, anadhani lina chakula. Mtu afanyae nyiradi zisizo na maana anaamini anapata ukaribu na Mungu, lakini kwa kweli yumo katika hali ya mdanganyiko. Fahamu zake zimepumbazika. Anafikiri kwamba amefikia hali ya kiroho ya juu, lakini kwa kweli hali ya moyo wake inabaki na uchafu. BURUDIKO KUTOKANA NA DHIKRI Mu Ahmadiyya mmoja mkweli wa moyo alipata kuniambia kwamba burudiko kubwa lapatikana katika matendo kama haya. Nilimwambia kwamba faraja hiyo inafanana na ile ipatikanayo kwa kutumia opium na cocaine. Ushahidi kamili ni kwamba Dhikr za aina hii hazileti usafi wa kiroho. Alikubali na akanieleza kuwa alimfahamu mtu mmoja aliyekuwa mahiri wa nyiradi zote hizo, lakini alikuwa akiomba omba chakula mitaani. Yule Mu-Ahmadiyya aliongeza kusema kwamba alikuwa akishangaa, kama mtu huyu amefikia hali ya juu ya kiroho anayoidai kwa nini anahitaji kuomba omba? Masihi Aliyeahidiwa (as) amesimulia hadithi ya mtu mmoja aliyedai kuwa ni mcha Mungu aliyefikia hali ya juu ya kiroho. Siku moja mtu huyu alimtembelea mfuasi wakekatika kipindi cha njaa, na akamdai “nipe karadha (hadhi) yangu”, yule mfuasi hakuwa nacho cha kumpa, hivyo akaomba asamehewe, lakini yule mtu aliendelea kusisitiza madai yake. Mwishowe yule mfuasi alilazimika kuuza baadhi ya vitu vyake vya ndani ili kukidhi madai ya mcha Mungu yule. Kwa kifupi mapungufu mengi na uchafu wa moyo vinaonekana kwa watu wanaojionyesha kama wameshakuwa wacha Mungu kwa njia potofu za Dhikri. TOFAUTI KATI YA DHIKRI NA ATHIRIKO TU LA MAWAZO Mungu Mwenye Enzi Ameweka katika sauti na mawazo ya binadamu nguvu maalum. Kama mtu ataendelea kufikiri kwamba jambo fulani limetokea basi akili yake itapatwa na athari hiyo hiyo. Vile vile, kama mtu anaanza kuwaza kwamba moyoni mwake anatoa sauti ya Allah, anaanza kuisikia sauti hiyo. Swali linazuka; kama moyo kweli unatoa sauti hiyo, kwa nini usitakaswe? Kuna tofauti ya muhimu kati ya wale ambao kweli wanampenda Mungu na wale wanaofanya ujanja tu. Tofauti ni rahisi, lakini kushindwa kuitambua kunamfanya mtu asijali kuhusu kujirekebisha. Anaweza kuamini kwamba amemfikia Allah, wakati kwa kweli hajamfikia. Kama mtu aliyefika mahali tofauti na alikokusudia kwenda, lakini akaamini amefika kwenye lengo lake, atakaa pale na kupata hasara yake. Wale wanaojiingiza katika matendo yaliyopotoka, wanadhani wamefikia lengo lao la kweli, lakini kwa kweli wako mbali nalo kwa maili nyingi. Kama ilivyo kwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, wako katika hali ya ganzi ya ulevi na pumbaziko la fahamu. Masihi Aliyeahidiwa (as) aliwahimiza wafuasi wake kukaa mbali na aina potofu za Dhikri. Aliwalaumu wale waliokuwa wakizifanya. “Inawezekanaje mambo haya yakaitwa kumbuko la Allah katika maana yake ya kweli ikiwa hata Wahindu na Wakristo wanaweza nao kuyatenda?” Alihoji KUTAMKA DHIKRI KWA SAUTI Vipi kuhusu kutamka Dhikri kwa sauti au kusikiliza nyimbo na muziki. Kama nilivyotaja mapema, mfumo wa neva wa binadamu umepewa nguvu ya kuathiri na vile vile kuathirika. Masikio yanatoa mojawapo ya njia zielekeazo kwenye mfumo wa neva. Husisimka kwa sauti zenye kuleta faraja. Hii inahusika sio tu kwa binadamu bali kwa viumbe vingine pia. Mpigie nyoka zumari na ataanza kucheza. Je utaweza kusema yupo kwenye athiriko la kiroho, la, bali ni hisia zake tu zimeathirika. Yeyote anayeamini kwamba kuimba kuna athari ya kiroho amekosea, kama ambavyo nyoka hucheza kufuata sauti ya zumari, vivyo hivyo Masufi wa leo husisimka kwa nyimbo na muziki. Zaidi ya hapo, ni bidaa katika imani ya Islam kufanya Dhikri kwa sauti. Masufi wa leo wanaenda kinyume na miongozo ya Mtume Mtukufu (saw) wanapofanyamkutano wa Dhikri, eneo lote walipo linajaa kelele. Wanadhania ni tendo la wema, wakati kwa kweli, wanaenda kinyume na ‘Sharia’ (sheria ya Islam). Matendo yao, kucheza, kupiga kelele, kuanguka, na kuzungusha vichwa vyao hayaendani na mafundisho ya Islam. JE MASHAIRI NI DHIKRI?

Description:
Dhikr-e -ilaahi au kumkumbuka Allah ni nini? - Kwa nini .. kulevya kama opium, cocaine na bangi zinaweza kupatikana kutokana na mkazio huu wa
See more

The list of books you might like

Most books are stored in the elastic cloud where traffic is expensive. For this reason, we have a limit on daily download.